Staftahi nikaimaliza na mara tu nilopoamka kutoka, nilipigwa na uzito wa wazo ya kuwa nilikuwa nimekuja kujiburudisha. Basi nilijiarifu kimoyomoyo nisiwe na haraka kamwe, aghalabu, kawaida ni kama sheria. Ni kawaida ya waswahili kutokuwa na haraka haraka zozote. Sote tumeziskia kawaida zao zisizo kasi. Utaratibu pasi harakati. Ni wanadamu wasiopenda kukimbia na nilijulishwa na boi mmoja kule ya kuwa sababu si joto jingi tu, bali mazoea tangu enzi.
Mhudumu yule aliponiona nimesimama dede, aliviringisha macho yake (ya kurembua). Ni kama kwayo alikuwa akinishangaa na kunionya ushamba wa bara niuwache kule. Isitoshe, nipo nchi ya pole, niende pole. "Unaondoka yakhe?" aliniuliza. "Naam" nilijikakamua kukisema kiswahili cha kuimba. "Aaah, kaka. Mbona hata chakula chenyewe hakijateremka?" . Nilitabasamu nakumpa ngano ya mkutano wa saa fulani, ambao nilishauchelewa. Aliniangalia juu chini kama kunipima na akijaribu kuficha kutoshawishika kwake, alinijibu "Haya basi, mapeni ni dala hamsini" huku akinipokeza cheti. Hamsa nikampa na kuuangalia mlango.
Jiji la mombasa si la kumpoteza yeyote, awe asiwe mgeni. Moja kwa moja niliondoka kueleka mji wa zamani ambao kwa sababu ya ziara za watalii wengi, umebatizwa na kubatizika old town. Old town kwa jumla ni kijiji wastani chenye nyumba zinazo hesabu jadi na karne kuzidi. Niliashiriwa na kuelezwa historia ya majumba; ya kifahari na yasiyo yaliyosimama kijijini. Urembo wayo kwa kweli ulikiwa kwenye miaka yao. Kwa ujenzi stadi na ufundi usioaminika (majumba yenyewe ni ya mbao na ya horofa!!). Kwa mpangilio unaozidi miji mingi ya kisasa. Si rahisi amakweli kueleza uzuri wa kijiji hicho kikamilifu.Nina arifa moja tu:Maji usiyoyafika, hujui wingi wake.