Naishi, natumaini
Najitolea daima Kenya, Hakika ya bendera
Ni udhabiti wangu, Nyeusi ya wananchi na
Nyekundu ni ya damu
Kijani ni ya ardhi, nyeupe ya amani
daima mimi mkenya, mwananchi mzalendo
Maneno haya si utenzi wangu mimi. Ni mwimbaji Eric Wainaina.
Nimekinai wimbo mwenyewe; kwani hadi sasa, hamna msanii mwingine ambaye ametupa kazi au wimbo ambao ni wa kizalendo na tena wenye kufikia kiwango cha kimataifa. Wimbo ambao ni wa kuburudisha na vilevile wenye ujumbe dhabiti - unaozungumzia wajibu wetu kama wananchi.
Mara ya kwanza kuusikia wimbo mwenyewe si juzi, la. Niliusikia miaka rudi - nikiwa shule ya upili papa hapa jijini nairobi. Kama wanakwaya shuleni, tulialikwa sherehe ya kutamatisha kibarua cha kukusanya mihela ambayou ingewaendea watoto waathiriwa kupunguza njaa humu nchini. Tulishinda njaa mchana kutwa na hela kiwango cha chakula cha mchana tukazikusanya. Tuliwapa wahisani tukitumaini na pia kuwaamini wazifikishe tulikokusudia.
Jioni baada ya haya yote, kijana mmoja ambaye wakati huo alikuwa akianzilia ulimwengu wa sanaa na uimbaji alikwea jukwaa. Kimya kilitanda mithili ya gubi gubi ya blankenti nzito alipoanza kuutirisha wimbo huu. Aliuimba kwa lugha ya kimombo na kwa kweli ungalilinganisha muziki wenyewe na mwingine wetu wakati huo, haungeamini ni utunzi na uimbaji wa mzaliwa.
Nisipoteze mada; wakenya lazima tuanze kujivunie ukwasi wetu wa lugha, wa utamaduni, wa manthari ya nchi, wa utaratibu wetu. Tusimame tisti, na kujivunia hali ii hii tuliyonayo. Tujivunie Kenya na Ukenya.
Video yenyewe: http://www.youtube.com/watch?v=TTzgA4t2Da0&feature=related
Saturday, March 28, 2009
Monday, March 16, 2009
Wikendi njema.
Sijui kwanza kama neno wikendi ni jina halisi la kiswahili. Hata hivyo, wikendi mbili zilizopita zimekuwa za kusisimua kweli (kwangu mimi inabidi niandike kuzihusu). Jumamosi nilikuwa upande wa Chuo Kikuu cha Nairobi ambopo nilikutana na akina dada wawili tulisoma pamoja mwaka ulopita. Mazungumzo yetu yalizuru hali nyingi za kuwepo lakini kwa kina, tuliyatafakari ya ujana na kumaliza shule. Ni kweli ujana tunao na tumeamua kama Wakenya wenzetu, na wa hali tofauti tofauti kutafuta ajira za kutukimu maisha. Kilichobakia mawazoni mwangu hata baada ya kuwapunga mkono wa buriani ni umuhimu wa "kujienjoy" (inavyosemekana kikenya!!) uki bado mchanga kwani kama ua, huja na kuenda.
Je, niulize; ujana una siri??? siri ya kujiendeleza ukiangalia siku za usoni?? ama ujana ni hali ya maisha tu, aipitiyae mja akieleke uzee (na uzee hapa ukiwa kukomaa na basi hali ya juu kabisa atakayoifikia mwanadamu)
Jumapili
Jumapili iliyofwatia nilikuwa nikitembea nje ya jengo la bunge ambapo nilimuona mzee mmoja kikongwe akipunga hewa chini ya ua moja la waridi. Niliamua kumsalimu mzee yule naye kanijibia kwa kimombo! (sikutarajia!!) Kuna kitu cha kupendeza azungumzapo mja wa makamo; macho yake yanayosimulia kuona mengi, sauti yake kuila chumvi na mawaidha yaliyojaa pomoni kwa kila neno alilolitamka. Alinipa mawazo mengi lakini ambalo lilibakia mawazoni mwangu tulipoagana ni ujasiri tunaouhitaji sisi vijana, ili tuweze kukaa pamoja kama wananchi toka sehemu na mienendo ya maisha tofauti kwa umoja.
Jumapili iliyofwatia baada ya ibada kanisani, niliamu kutembea polepole kuelekea nyumbani. (Niliamua kupitia kwenye duka la rejareja la Tuskys, barabara ya Biashara. Sikuwa na hila bayana bali nilipoona maji ya matunda yakiuzwa niliamua kujinunulia ya machungwa na nanasi mchanganyiko.) Nikiivutia mrija pole pole, nilitafakari yaliyofunzwa Kanisani; ya kuwa ibada yake mwenyezi Mungu ndilo jukumu fika la mwanadamu - hapana lingine.
Haya yote nikiyang'amua, na kuyatafakari kwa jumla na nikafikia mwisho wa jambo hili, jukumu letu waja ni kumcha Mungu, mengine yapo hapa na pale.
Thursday, March 12, 2009
Taarab
Kwa wapenzi wa lugha, nimejivumbulia starehe iliyoswafi na tena yenye kuburudisha: TAARAB.
Kulingana na hadithi zinazoenea pwani hadi Zanzibari, muziki wenyewe ulianzilishwa na Sultani Seyyid Barghash bin Said ambaye alijulikana kwa mapenzi yake ya maisha; na kwa maisha yake ya raha mstarehe. Alikisafirisha kikundi kimoja kutoka Misri ili waweze kumchezea taarabl-nyimbo zilizoimbwa kwa lugha ya kiarabu-kwenye Kasri lake Beit-al-Ajab (amakweli alikuwa mstarehe sultan!) .
Ladba umemsikia Siti Bint Saad? mwimbaji aliyevuma sifa Zanzi miaka ya nyuma. Siti, ambaye jina lake alipewa kwa kuwa dada taratibu sana, alijifunza uimbaji akiwa mchanga. Alianza na nyimbo za wakati wake, na kuendelea kujivumbulia utaratibu mpya hata kuzitafsiri nyimbo zenyewe kwa kiswahili. Dada hodari amekuwa changamoto kubwa kwa taarab tunavyoijua leo; mengineyo si ya dharura?
Kipindi cha Rusha Roho, ambacho hupeperushwa kila Jumapili kuanzia saa tisa kamili hadi saa moja za jioni, nilikigundua kibahati na sibu. Katika masafa ya mia moja na kitu nukta, radio citizen basi huwa ndio mpangilio. Nyimbo kama vile paka mapepe na nyinginezo (kumradhi nazijifunza bado!) hushauri, hukejeli, huelimisha na huburudisha unono. Kuna dada fulani pia kwenye masafa tofauti wakati uo huo ambaye pia hupeperusha nyimbo za uswahilini fika. (Utafurahia umalenga stadi ulio kawaida ya nyimbo hizi)
Kiswahili chake Hasan, ambaye ndiye nahodha wa Rusha Roho pia ni cha kusisimua. Hata ukawa wewe mgeni tu, na kumsikiza ni kwa mara ya kwanza, utafurahia. Kipya kinyemi kisicho kidonda. Maneno yake huyachagua kwa ustadi usiodhahiri, na pia ni jamaa mwenye raha tele; utapenda.
Sijui kama nimekushawishi fika? Kwangu mimi, tukitukuze kiswahili.
Sunday, March 1, 2009
Dhamira badala
Kawaida ya waja ni ziendapo mawazo, hufwata kama bendera upepo. Nami nimesadiki, afua ni mbili - kufa na kupona. Aidha uende mbele au urudi nyuma, ufurahi au ujae simanzi...mifano i kote kote. Siku yangu ilinusurika kuharibika baada ya kuketi kwenye kiti kimoja cha umma. Basi akaja boi mmoja akaketi kando yangu. Sikufikiria lolote; si haki ya yeyote kujipumzisha hapa?
Mara, kijana akachomoa kibeti chake chenye mihela iliyopangwa kunyooka mithili ya askari gwarideni. Huku akiniangalia kwenye ncha la jicho, alianza kupiga binja. Nilipendua sura na kuangazia pengine. Kidogo, akakitia kibeti kwenye paja na kuanza kusema kiingereza cha puani. "Hello, hev you delivered the fen?", "no, no, no,no it need installed now!" majigambo ya wapwani? sikufahamu. Nakangazia pengine, wakati huu mbali zaidi.
Ni kwa kasi za umeme jamaa yule alipogutuka na kuchomoka pale kitini. Moja kwa moja alielekea asiangalie nyuma. Kibeti chake kikaanguka naye ameukaza mwendo. "Ali!" nikamuita jina la jumla ( na la heshima) aitwalo yeyote usiyemjua naye amezingatia kijia kana kwamba ardhi itafunga safari wakati wowote sasa. "Ali we!" hakupenduka bali aliendelea hadi kipeo cha macho, nisimuone tena. Kila mmoja aliyekuwa ameketi pale alijifanya ni kama hakuna lolote lililoendelea.
Akomapo mwenyeji na mgeni koma. Nilisimama kwa utaratibu, na kutoka pale. Sikuwa nimeenda umbali wa sikio kusikia ndipo nikawasikia wale walioketi pale wakisema- mwerevu huyu po! angalinaswa na mtego na hakuwemo. Ni ujanja au ilikuwa ni kweli? nilijiuliza na kukinai, dhamira ya kusaidia wakati mwingine utaibadilisha.
Subscribe to:
Posts (Atom)