Monday, March 16, 2009

Wikendi njema.

Sijui kwanza kama neno wikendi ni jina halisi la kiswahili. Hata hivyo, wikendi mbili zilizopita zimekuwa za kusisimua kweli (kwangu mimi inabidi niandike kuzihusu). Jumamosi nilikuwa upande wa Chuo Kikuu cha Nairobi ambopo nilikutana na akina dada wawili tulisoma pamoja mwaka ulopita. Mazungumzo yetu yalizuru hali nyingi za kuwepo lakini kwa kina, tuliyatafakari ya ujana na kumaliza shule. Ni kweli ujana tunao na tumeamua kama Wakenya wenzetu, na wa hali tofauti tofauti kutafuta ajira za kutukimu maisha. Kilichobakia mawazoni mwangu hata baada ya kuwapunga mkono wa buriani ni umuhimu wa "kujienjoy" (inavyosemekana kikenya!!) uki bado mchanga kwani kama ua, huja na kuenda.

Je, niulize; ujana una siri??? siri ya kujiendeleza ukiangalia siku za usoni?? ama ujana ni hali ya maisha tu, aipitiyae mja akieleke uzee (na uzee hapa ukiwa kukomaa na basi hali ya juu kabisa atakayoifikia mwanadamu)
Jumapili
Jumapili iliyofwatia nilikuwa nikitembea nje ya jengo la bunge ambapo nilimuona mzee mmoja kikongwe akipunga hewa chini ya ua moja la waridi. Niliamua kumsalimu mzee yule naye kanijibia kwa kimombo! (sikutarajia!!) Kuna kitu cha kupendeza azungumzapo mja wa makamo; macho yake yanayosimulia kuona mengi, sauti yake kuila chumvi na mawaidha yaliyojaa pomoni kwa kila neno alilolitamka. Alinipa mawazo mengi lakini ambalo lilibakia mawazoni mwangu tulipoagana ni ujasiri tunaouhitaji sisi vijana, ili tuweze kukaa pamoja kama wananchi toka sehemu na mienendo ya maisha tofauti kwa umoja.

Jumapili iliyofwatia baada ya ibada kanisani, niliamu kutembea polepole kuelekea nyumbani. (Niliamua kupitia kwenye duka la rejareja la Tuskys, barabara ya Biashara. Sikuwa na hila bayana bali nilipoona maji ya matunda yakiuzwa niliamua kujinunulia ya machungwa na nanasi mchanganyiko.) Nikiivutia mrija pole pole, nilitafakari yaliyofunzwa Kanisani; ya kuwa ibada yake mwenyezi Mungu ndilo jukumu fika la mwanadamu - hapana lingine.
Haya yote nikiyang'amua, na kuyatafakari kwa jumla na nikafikia mwisho wa jambo hili, jukumu letu waja ni kumcha Mungu, mengine yapo hapa na pale.

2 comments:

  1. "Kiswahili kitukuzwe". Wahenga walisema. Ni bayana kuwa hawakukosea. Nakushuru Allan kwa kutumia lugha hii kwa mtandao huu wako wa blog. Nimetambua ya kwamba ni upesi sana kujichanganya ukitafakari vyenye lugha yenyewe imeshambuliwa na vijana kwa kutumia maneno ya mtaani- "Sheng".

    ReplyDelete
  2. @James'

    Aksante kwa maoni yako, nashukuru.

    Kwa kweli ni vigumu kutunza kitu kama lugha au utamaduni wetu bila ya sisi wenyewe kuchukua jukumu na kufanya hili au lile. Bila ya kukitumia kitu, utakipoteza. Ni mara ngapi nimekutana na watu amboa kwa mfano wamelipa hela nyingi kujifunza lugha ya kigeni; na baada ya muda mfupi wamekisahau chote!Si vibaya kujifunza lugha za kigeni, lakini wasemavyo, akili nyingi huondoa maarifa. Maarifa hapa, ni tutumie lugha tuliyonayo, kisha tuendelee na zinginezo. Fimbo ya karibu ndiyo imuuwaye nyoka.

    Sheng' sasa imekuwa ni lugha mmpya na hapana njia itakayositiriwa. Kwa maoni yangu, kwa kuwa wengi wanaipenda, na iwe. Ama?

    ReplyDelete