Monday, February 23, 2009

ziwa, madafu na zaidi

Jiji ni la Mombasa... Safari yangu niliifunga toka Nairobi kuelekea  baada ya kukimaliza kibarua fulani katika shirika la Kenya ICT Board. Usiku wa safari ulikua ni mtulivu, mwanana hata; nami nilijawa bashasha mpwito. Tuliondoka saa nne kasorobo za usiku na kama kawaida, usinginzi ulinichukua mara tu nilipoingia kwenye basi, kuketi na kuuhisi ubembeo wa mwenendo. Nyweee....safari hiyo, na mara nilipozinduka, joto nisilolizoa lilitanda kote - hewa iliyojawa kijiharufu cha chumvi ikanijia, ndipo nikagundua nipo pwani.

Wakati huu, jua lilikuwa lishazuka. Mandhari ya pwani kama nilivyotaraji yalitawaliwa na minazi iliyoyumba kwa upepo mithili ya wachezaji stadi wanapovilegeza viungo katika ngoma, mbumbumbu haswa. Mawazo yangu yalinipeleka mbali sana, mwaka wa tisini na nane ambao ulikuwa ni mwaka wangu wa mwisho kulitembelea jiji hili.

Basi, kajifanya mwenyeji, nikatoka moja kwa moja kwenye kituo cha mabasi kuelekea jijini. Harufu nzuri ya kukaanga viazi, mihogo na mapocho tofauti ya uswahilini ilinijia na kunitosamo nisiweze kuupita mkahawa (nafikiri Mvita Hotel), uliokuwa bayana kwangu kama chanzo cha vizuri hivyo. Waswahili husema kama tamu inaua, basi na sumu kazi yake nini? Nilisalimu amri na kusema kweli, tamu yazo pocho pocho siisahau asilani.

Washikaji, hekaya zangu pwani (na zinginezo) basi ziangalieni papa hapa, nikikamilisha masalio ya siku hiyo, na za siku zilizofwatia. Mombasa, masalaala.......raha?!

2 comments:

  1. blogging in swahili is a step in new direction. Keep it up!

    ReplyDelete
  2. La Vida,

    Shukrani. Sijui uliigunduaje kurasa hii ya kiswahili lakini hata hivyo, ni vyema. Ningeomba maoni yako zaidi; haswa kwa kuwa naona wewe ni mwenyeji katika dunia hii ya kuandika mtandaoni.
    Ningependa unifafanulie kwa hisani yako, muelekeo huu mpya unaougusia katika oni lako hapo juu.

    ReplyDelete