Wednesday, June 3, 2009

Mwerevu huling'amua

Fumbo mfumbie mjinga.

Mawazo yangu ya karibuni yanielekeza siku za usoni. Angalau jana kashakwenda sirudi, ganda la muwa la jana chungu kaona kivuno.

Mara kwa mara nimesikia ya kwamba ukitaka kutabiri ya kesho, tazama jana. Pinda shingo utazame yaliyokwisha tendeka na kwayo, utapata maono yasiyopatikana pengine popote. Kwa muda uliosalia, tafakari ya kuwa:

1. Kupotea njia ndiko kujua njia

2. Hiari yashinda utumwa

3. Kila chombo kwa wimbile


Hapana kitu cha fahari tulichonacho waja ila muda. Ni bora tufahamu njia na nia, na MUDA wake.

Monday, April 13, 2009

Havitatajwa fedhaluka wala bilauri

Hakika kuna shimo wachimbako fedha, na mahali wapatapo dhahabu waisafishayo. Chuma hufunikwa katika ardhi,na shaba huyeyushwa katika mawe. Binadamu hukomesha giza;huyatafutatafuta hata mpaka ulio mbali, mawe ya giza kuu, giza tupu.

Hufikia shimo mbali na makao ya watu; palikosahaulika na nyayo zipitazo. Hining'inia mbali na watu, huyumba-yumba huko na huko. Katika ardhi ndimo kitokeamo chakula; na chini yake hupinduliwa kama kwa moto. Mawe yake ni mahali zipatikanapo yakuti; nayo ina mchanga wa dhahabu.

Njia ile hapana ndege mkali aijuaye, wala jicho la tai halijaiona. Wanyama wakali wajivunao hawajaikanyaga, wala simba mkali hajaipita. Huunyoshea mwamba wa gume gume mkono wake, huipindua milima hata misingi yake. Hukata mifereji kati ya majabali,Na jicho Lake huona kila kitu cha thamani. Hufunga vijito visichuruzike; na kitu kilichostirika hukifunua.

Bali hekima itapatikana wapi, mahali pa ufahamu ni wapi?

Mwanadamu hajui thamani yake, wala haionekani katika nchi ya walio hai.

Vilindi vyasema, "Haimo ndani yangu"
Na bahari yasema, "Haiko kwangu"

Haipatikani kwa dhahabu, wala fedha haitapimwa iwe thamani yake. Haiwezi kutiwa thamani kwa dhahabu ya Ofiri. Wala kwa shohamu ya thamani nyingi, wala kwa yakuti ya samawi.

Dhahabu na vioo haiwezi kulinganishwa nayo; wala kubadili kwake hakutakuwa kwa vyombo vya dhahabu safi. Havitatajwa fedhaluka wala bilauri; Naam Kima cha hekima chapita marijani. Yakuti ya rangi ya manjano ya kushi haitasawazishwa nayo, wala haitatiwa kima kwa dhahabu safi.

Basi hekima yatoka wapi? kwa kuwa imefichwa mbali na macho ya wote walio hai, na kusitirika na ndege wa angani. Uharibifu na mauti husema, "tumesikia habari zake kwa masikio yetu."

Mungu ndiye aijuaye njia yake, Naye ajua mahali pake. Maana anatazama hata miisho ya nchi, na kuona chini ya mbingu nzima. Apate kuufanyia upepo uzito wake; naam anayepima maji kwa kipimo. Hapo alipoiwekea mvua amri, na njia kwa umeme wa radi. Ndipo alipoiona na kuitangaza; aliidhibitisha, naam na kuichunguza.

Kisha, akamwambia mwanadamu: Tazama, kumcha Bwana ndiyo hekima. Na kujitenga na uovu ndio ufahamu

Saturday, March 28, 2009

Mkenya Mzalendo

Naishi, natumaini
Najitolea daima Kenya, Hakika ya bendera
Ni udhabiti wangu, Nyeusi ya wananchi na
Nyekundu ni ya damu
Kijani ni ya ardhi, nyeupe ya amani
daima mimi mkenya, mwananchi mzalendo

Maneno haya si utenzi wangu mimi. Ni mwimbaji Eric Wainaina.

Nimekinai wimbo mwenyewe; kwani hadi sasa, hamna msanii mwingine ambaye ametupa kazi au wimbo ambao ni wa kizalendo na tena wenye kufikia kiwango cha kimataifa. Wimbo ambao ni wa kuburudisha na vilevile wenye ujumbe dhabiti - unaozungumzia wajibu wetu kama wananchi.

Mara ya kwanza kuusikia wimbo mwenyewe si juzi, la. Niliusikia miaka rudi - nikiwa shule ya upili papa hapa jijini nairobi. Kama wanakwaya shuleni, tulialikwa sherehe ya kutamatisha kibarua cha kukusanya mihela ambayou ingewaendea watoto waathiriwa kupunguza njaa humu nchini. Tulishinda njaa mchana kutwa na hela kiwango cha chakula cha mchana tukazikusanya. Tuliwapa wahisani tukitumaini na pia kuwaamini wazifikishe tulikokusudia.

Jioni baada ya haya yote, kijana mmoja ambaye wakati huo alikuwa akianzilia ulimwengu wa sanaa na uimbaji alikwea jukwaa. Kimya kilitanda mithili ya gubi gubi ya blankenti nzito alipoanza kuutirisha wimbo huu. Aliuimba kwa lugha ya kimombo na kwa kweli ungalilinganisha muziki wenyewe na mwingine wetu wakati huo, haungeamini ni utunzi na uimbaji wa mzaliwa.

Nisipoteze mada; wakenya lazima tuanze kujivunie ukwasi wetu wa lugha, wa utamaduni, wa manthari ya nchi, wa utaratibu wetu. Tusimame tisti, na kujivunia hali ii hii tuliyonayo. Tujivunie Kenya na Ukenya.

Video yenyewe: http://www.youtube.com/watch?v=TTzgA4t2Da0&feature=related

Monday, March 16, 2009

Wikendi njema.

Sijui kwanza kama neno wikendi ni jina halisi la kiswahili. Hata hivyo, wikendi mbili zilizopita zimekuwa za kusisimua kweli (kwangu mimi inabidi niandike kuzihusu). Jumamosi nilikuwa upande wa Chuo Kikuu cha Nairobi ambopo nilikutana na akina dada wawili tulisoma pamoja mwaka ulopita. Mazungumzo yetu yalizuru hali nyingi za kuwepo lakini kwa kina, tuliyatafakari ya ujana na kumaliza shule. Ni kweli ujana tunao na tumeamua kama Wakenya wenzetu, na wa hali tofauti tofauti kutafuta ajira za kutukimu maisha. Kilichobakia mawazoni mwangu hata baada ya kuwapunga mkono wa buriani ni umuhimu wa "kujienjoy" (inavyosemekana kikenya!!) uki bado mchanga kwani kama ua, huja na kuenda.

Je, niulize; ujana una siri??? siri ya kujiendeleza ukiangalia siku za usoni?? ama ujana ni hali ya maisha tu, aipitiyae mja akieleke uzee (na uzee hapa ukiwa kukomaa na basi hali ya juu kabisa atakayoifikia mwanadamu)
Jumapili
Jumapili iliyofwatia nilikuwa nikitembea nje ya jengo la bunge ambapo nilimuona mzee mmoja kikongwe akipunga hewa chini ya ua moja la waridi. Niliamua kumsalimu mzee yule naye kanijibia kwa kimombo! (sikutarajia!!) Kuna kitu cha kupendeza azungumzapo mja wa makamo; macho yake yanayosimulia kuona mengi, sauti yake kuila chumvi na mawaidha yaliyojaa pomoni kwa kila neno alilolitamka. Alinipa mawazo mengi lakini ambalo lilibakia mawazoni mwangu tulipoagana ni ujasiri tunaouhitaji sisi vijana, ili tuweze kukaa pamoja kama wananchi toka sehemu na mienendo ya maisha tofauti kwa umoja.

Jumapili iliyofwatia baada ya ibada kanisani, niliamu kutembea polepole kuelekea nyumbani. (Niliamua kupitia kwenye duka la rejareja la Tuskys, barabara ya Biashara. Sikuwa na hila bayana bali nilipoona maji ya matunda yakiuzwa niliamua kujinunulia ya machungwa na nanasi mchanganyiko.) Nikiivutia mrija pole pole, nilitafakari yaliyofunzwa Kanisani; ya kuwa ibada yake mwenyezi Mungu ndilo jukumu fika la mwanadamu - hapana lingine.
Haya yote nikiyang'amua, na kuyatafakari kwa jumla na nikafikia mwisho wa jambo hili, jukumu letu waja ni kumcha Mungu, mengine yapo hapa na pale.

Thursday, March 12, 2009

Taarab

Kwa wapenzi wa lugha, nimejivumbulia starehe iliyoswafi na tena yenye kuburudisha: TAARAB.

Kulingana na hadithi zinazoenea pwani hadi Zanzibari, muziki wenyewe  ulianzilishwa na Sultani Seyyid Barghash bin Said ambaye alijulikana kwa mapenzi yake ya maisha;  na kwa maisha yake ya raha  mstarehe. Alikisafirisha kikundi kimoja kutoka Misri ili waweze kumchezea taarabl-nyimbo zilizoimbwa kwa lugha ya kiarabu-kwenye Kasri lake Beit-al-Ajab (amakweli alikuwa mstarehe sultan!) .

Ladba umemsikia Siti Bint Saad? mwimbaji aliyevuma sifa Zanzi miaka ya nyuma. Siti, ambaye jina lake alipewa kwa kuwa dada taratibu sana, alijifunza uimbaji akiwa mchanga. Alianza na nyimbo za wakati wake, na kuendelea kujivumbulia utaratibu mpya hata kuzitafsiri nyimbo zenyewe kwa kiswahili. Dada hodari amekuwa changamoto kubwa kwa taarab tunavyoijua leo; mengineyo si ya dharura?

Kipindi cha Rusha Roho, ambacho hupeperushwa kila Jumapili kuanzia saa tisa kamili hadi saa moja za jioni, nilikigundua kibahati na sibu. Katika masafa ya mia moja na kitu nukta, radio citizen basi huwa ndio mpangilio. Nyimbo kama vile paka mapepe na nyinginezo (kumradhi nazijifunza bado!) hushauri, hukejeli, huelimisha na  huburudisha unono. Kuna dada fulani pia kwenye masafa tofauti wakati uo huo ambaye pia hupeperusha nyimbo za uswahilini fika. (Utafurahia umalenga stadi ulio kawaida ya nyimbo hizi)

Kiswahili chake Hasan, ambaye ndiye nahodha wa Rusha Roho pia ni cha kusisimua. Hata ukawa wewe mgeni tu, na kumsikiza ni kwa mara ya kwanza, utafurahia. Kipya kinyemi kisicho kidonda. Maneno yake huyachagua kwa ustadi  usiodhahiri, na pia ni jamaa mwenye raha tele; utapenda.

Sijui kama nimekushawishi fika? Kwangu mimi, tukitukuze kiswahili.

Sunday, March 1, 2009

Dhamira badala

Kawaida ya waja ni ziendapo mawazo, hufwata kama bendera upepo. Nami nimesadiki, afua ni mbili - kufa na kupona. Aidha uende mbele au urudi nyuma, ufurahi au ujae simanzi...mifano i kote kote. Siku yangu ilinusurika kuharibika baada ya kuketi kwenye kiti kimoja cha umma. Basi akaja boi mmoja akaketi kando yangu. Sikufikiria lolote; si haki ya yeyote kujipumzisha hapa? 

Mara, kijana  akachomoa kibeti chake chenye mihela iliyopangwa kunyooka mithili ya askari gwarideni. Huku akiniangalia kwenye ncha la jicho, alianza kupiga binja. Nilipendua sura na kuangazia pengine. Kidogo, akakitia kibeti kwenye paja na kuanza kusema kiingereza cha puani. "Hello, hev you delivered the fen?", "no, no, no,no it need installed now!" majigambo ya wapwani? sikufahamu. Nakangazia pengine, wakati huu mbali zaidi. 

Ni kwa kasi za umeme jamaa yule alipogutuka na kuchomoka pale kitini.  Moja kwa moja alielekea asiangalie nyuma. Kibeti chake kikaanguka naye ameukaza mwendo. "Ali!" nikamuita jina la jumla ( na la heshima) aitwalo yeyote usiyemjua naye amezingatia kijia kana kwamba ardhi itafunga safari wakati wowote sasa. "Ali we!" hakupenduka bali aliendelea hadi kipeo cha macho, nisimuone tena. Kila mmoja aliyekuwa ameketi pale alijifanya ni kama hakuna lolote lililoendelea. 

Akomapo mwenyeji na mgeni koma. Nilisimama kwa utaratibu, na kutoka pale. Sikuwa nimeenda umbali wa sikio kusikia ndipo nikawasikia wale walioketi pale wakisema- mwerevu huyu po! angalinaswa na mtego na hakuwemo. Ni ujanja au ilikuwa ni kweli? nilijiuliza na kukinai, dhamira ya kusaidia wakati mwingine utaibadilisha.

Monday, February 23, 2009

Mji wa zamani

Staftahi nikaimaliza  na mara tu nilopoamka kutoka, nilipigwa na uzito wa wazo ya kuwa nilikuwa nimekuja kujiburudisha. Basi nilijiarifu kimoyomoyo nisiwe na haraka kamwe, aghalabu, kawaida ni kama sheria. Ni kawaida ya waswahili kutokuwa na haraka haraka zozote. Sote tumeziskia kawaida zao zisizo kasi.  Utaratibu pasi harakati. Ni wanadamu wasiopenda kukimbia na nilijulishwa na boi mmoja kule ya kuwa sababu si joto jingi tu, bali mazoea tangu enzi.

Mhudumu yule aliponiona nimesimama dede, aliviringisha macho yake (ya kurembua). Ni kama kwayo alikuwa akinishangaa na kunionya ushamba wa bara niuwache kule. Isitoshe, nipo nchi ya pole, niende pole. "Unaondoka yakhe?" aliniuliza. "Naam" nilijikakamua kukisema kiswahili cha kuimba. "Aaah, kaka. Mbona hata chakula chenyewe hakijateremka?" . Nilitabasamu nakumpa ngano ya mkutano wa saa fulani, ambao nilishauchelewa. Aliniangalia juu chini kama kunipima na akijaribu kuficha kutoshawishika kwake, alinijibu "Haya basi, mapeni ni dala hamsini" huku akinipokeza cheti. Hamsa nikampa na kuuangalia mlango.

Jiji la mombasa si la kumpoteza yeyote, awe asiwe mgeni.  Moja kwa moja niliondoka kueleka mji wa zamani ambao kwa sababu ya ziara za watalii wengi, umebatizwa na kubatizika old town. Old town kwa jumla ni kijiji wastani chenye nyumba zinazo hesabu jadi na karne kuzidi. Niliashiriwa na kuelezwa historia ya majumba; ya kifahari na yasiyo yaliyosimama kijijini. Urembo wayo kwa kweli ulikiwa kwenye miaka yao. Kwa ujenzi stadi na ufundi usioaminika (majumba yenyewe ni ya mbao na ya horofa!!).  Kwa mpangilio unaozidi miji mingi  ya kisasa. Si rahisi amakweli kueleza uzuri wa kijiji hicho kikamilifu.Nina arifa moja tu:Maji usiyoyafika, hujui wingi wake.

ziwa, madafu na zaidi

Jiji ni la Mombasa... Safari yangu niliifunga toka Nairobi kuelekea  baada ya kukimaliza kibarua fulani katika shirika la Kenya ICT Board. Usiku wa safari ulikua ni mtulivu, mwanana hata; nami nilijawa bashasha mpwito. Tuliondoka saa nne kasorobo za usiku na kama kawaida, usinginzi ulinichukua mara tu nilipoingia kwenye basi, kuketi na kuuhisi ubembeo wa mwenendo. Nyweee....safari hiyo, na mara nilipozinduka, joto nisilolizoa lilitanda kote - hewa iliyojawa kijiharufu cha chumvi ikanijia, ndipo nikagundua nipo pwani.

Wakati huu, jua lilikuwa lishazuka. Mandhari ya pwani kama nilivyotaraji yalitawaliwa na minazi iliyoyumba kwa upepo mithili ya wachezaji stadi wanapovilegeza viungo katika ngoma, mbumbumbu haswa. Mawazo yangu yalinipeleka mbali sana, mwaka wa tisini na nane ambao ulikuwa ni mwaka wangu wa mwisho kulitembelea jiji hili.

Basi, kajifanya mwenyeji, nikatoka moja kwa moja kwenye kituo cha mabasi kuelekea jijini. Harufu nzuri ya kukaanga viazi, mihogo na mapocho tofauti ya uswahilini ilinijia na kunitosamo nisiweze kuupita mkahawa (nafikiri Mvita Hotel), uliokuwa bayana kwangu kama chanzo cha vizuri hivyo. Waswahili husema kama tamu inaua, basi na sumu kazi yake nini? Nilisalimu amri na kusema kweli, tamu yazo pocho pocho siisahau asilani.

Washikaji, hekaya zangu pwani (na zinginezo) basi ziangalieni papa hapa, nikikamilisha masalio ya siku hiyo, na za siku zilizofwatia. Mombasa, masalaala.......raha?!